Thursday, December 5, 2024
Home > Sports News > Ronaldo alivyoandikisha historia na orodha ya mechi za leo

Ronaldo alivyoandikisha historia na orodha ya mechi za leo

Cristiano Ronaldo asherehekea bao lake la kwanza dhidi ya Uhispania

Cristiano Ronaldo alifunga mabao matatu hiyo jana katika ngarambe ya funga-nifunge, ambapo Ureno ilitoka sare ya mabao matatu na Uhispania. Bao la kwanza la Ronaldo lilikuwa mkwaju wa penalti baada ya kutegwa kwenye msambamba. Mshambulizi huyo aliyebobea katika upigaji wa penalti alifunga kwa ustadi, kwani aliweka mpira kulia naye David De Gea akaenda kushoto.

 

Hata hivyo, uongozi wa Ureno haukudumu muda mrefu maadam Isco alimwandalia Diego Costa pasi maridadi, akawakanganya walinzi wa Ureno na kutia mpira wavuni. Mechi hiyo iliyokuwa na msisimko wa aina yake ilisheheni mashambulizi kadha ya kushtukiza, huku kila timu ikihitajika kuwa makini. Dakika moja kabla ya mapumziko, Ureno waliandaa shambulizi la kushtukiza na licha ya kuwa walinzi wa Uhispania walikuwa wamerejea maskanini, Ronaldo alipenyeza shuti lake lililomshinda kipa De Gea na mpira ukabingiria ndani.

Kipa David De Gea (jezi ya kijani) , JordiAlba(18) na Gerard Pique (3) wakijaribu kumzuia Ronaldo

 

Kipindi cha pili kilishuhudia mihemko si haba, Diego Costa akisawazishia Hispania dakika ya hamsini na tatu kwa ukamilifu stadi naye Nacho akaongeza la tatu dakika tano baadaye kwa shuti la mbali. Hatua hiyo illipa Uhispania uongozi wa mechi hiyo kwa takriban dakika thelathini kabla ya Ronaldo kuwaadhibu tena.

Kwa mara nyingine Sergio Bousquets alimwangusha Cristiano nje ya msambamba na kumlazimu refarii kuwatunuku Ureno mkwaju wa fauli mita thelathini kutoka kwa goli. Kama ilivyo ada, Ronaldo alichukua jukumu la upigaji, na baada ya kuvuta pumzi mara tatu alivurumisha kiki la kiaina lililomlazimu De Gea kusimama na kutazama mpira ukijaa wavuni. Ronaldo sasa ndiye mchezaji mkongwe zaidi kufunga mabao matatu kwa mechi moja kwa kombe hili la dunia, na wa kwanza tamgu mechi hizo zianze Alhamisi.

Mohamed Elneny na mwenzake wa Misri (jezi nyekundu) wasononeka baada ya kupigwa bao dakika ya tisini na Uruguay

Awali, Morroco walio kwenye kundi moja na Ureno na Uhispania, walipoteza kwa bao moja dhidi ya Iran wanaoongoza kundi hilo kwa sasa. Katika mechi nyingine iliyohusisha taifa la Afrika, Misri ilipigwa bao la uchungu dakika ya tisini na Jose Gimenez wa Uruguay katika kisa cha msumari wa mwisho.

Wachezaji wa Iran baada ya ushindi wao dhidi ya Morocco

Michuano kadhaa itaandaliwa leo vilevile na itahusisha Kundi C na D; Ufaransa itachuana na Australia saa saba mchana, kabla ya Argentina kugaragaza Iceland saa kumi alasiri. Saa moja usiku itakuwa zamu ya Peru na Denmark, huku Croatia na Nigeria zikikunja jamvi la mechi za leo saa nne usiku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *